Baraza hilo limetoa tangazo hilo leo Jumapili, siku moja baada ya Marekani kufanya mashambulizi makubwa ya kijeshi katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a na mikoa ya Sa'ada, Dhamar, Hajjah na al-Bayda.
Kwa akali watu 31, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, waliuawa katika mashambulizi hayo ya anga na majini yaliyoagizwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Baraza hilo limesema kuwa, kuwalenga raia kunathibitisha kushindwa kwa Marekani katika makabiliano hayo na kuongeza kuwa, uchokozi huo hautawazuia Wayemeni kuunga mkono Gaza, na badala yake utazidisha taharuki.
"Adhabu ya wavamizi dhidi ya Yemen itatekelezwa kwa weledi na uchungu, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu," limeonya Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen. Baraza hilo pia limebainisha kuwa, mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen yanaashiria kurejea kwa operesheni za kijeshi katika Bahari ya Shamu, na hivyo kuwa tishio kwa safari za kimataifa za baharini katika eneo hilo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Marekani, pamoja na utawala wa Kizayuni, watashindwa na kurudi nyuma kwa fedheha na udhalili, kama walivyofanya wakati wa vita vyao vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Imeongeza kuwa, "Yemen itasimama kidte na kuendelea kuunga mkono na kuisaidia Palestina; na kwamba operesheni za jeshi la majini zitaendelea hadi mzingiro wa Gaza utakapoondolewa, na msaada wa kibinadamu kuruhusiwa kuingia."
342/
Your Comment